Jan 18, 2021 11:52 UTC
  • Rwanda na Malawi zafunga shule tena baada ya maambukizo ya corona kuongezeka

Serikali za Rwanda na Malawi kuanzia leo Jumatatu zimefunga shule zikiwemo za chekechea kutokana na ongezeko la kesi za maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 katika nchi hizo.

Wizara ya Elimu ya Rwanda imesema kuwa, shule zilizofungwa kuanzia leo ni zile tu za mji mkuu Kigali, na kwamba ikilizamu serikali itafunga hata zile za miji na mikoa mingine.

Rwanda ilifungua shule zote za nchi hiyo mwezi Novemba mwaka uliopita, baada ya maambukizo ya corona kupungua. Machi 15 mwaka jana, serikali ya Rwanda ilitangaza kuchukua hatua kadhaa za dharura kukabiliana na janga la virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa shule zote za umma na za kibinafsi.

Mwezi uliopita, Waziri wa Afya wa Rwanda, Daniel Ngamije alionya kuwa maambukizi ya COVID-19 nchini Rwanda yalikuwa yamefika kiwango cha hatari kutokana na ongezeko la maambukizi na vifo. Hadi sasa watu 11,000 wameambukizwa Covid-19 nchini Rwanda huku waliofariki dunia wakipindukia 140.

Wanafunzi wakiwa shuleni nchini Rwanda

Malawi kwa upande wake imetangaza kuwa imefunga shule zote kuanzia leo Jumatatu, na hali hii itaendelea angalau kwa siku 15. Nchi hiyo imechukua hatua hiyo pamoja na nyingine kadhaa za kuzuia msambao wa virusi vya corona, baada ya kuongezeka kesi za maambukizi na vifo vya corona. 

Nchi hiyo haikunakili kesi yoyote ya Covid-19 katika kipindi cha miezi miwili, lakini imeshuhudia ongezeko la kutisha ndani ya siku chache zilizopita. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Malawi, nchi hiyo kufikia sasa imerekodi kesi 12,000 za corona mbali na vifo 300, huku thuluthi moja ya vifo hivyo vikiripotiwa ndani ya siku 16 zilizopita.

Kwa ujumla, bara la Afrika hadi sasa limenakili kesi milioni 3.1 za corona, huku wagonjwa 76,000 wa Covid-19 wakiaga dunia barani humo.

Tags