Jan 19, 2021 02:36 UTC
  • Marekani yakamilisha mpango wa kuwaondoa askari wake nchini Somalia

Marekani imetangaza kuwa, imekamilisha mpango wa kuwaondoa askari wake waliokuwa nchini Somalia.

Hayo yameelezwa na kanali Chris Karns msemaji wa Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM ambaye amebainisha kwamba, mpango wa kuwaondoa askari hao nchini Somalia umekamilika kabla ya muda wa mwisho uliokuwa umeainishwa hapo kabla.

Aidha amesema, katika hatua ya awali askari hao wamepelekwa katika nchi nyingine za Kiafrika zilizokko jirani na Somalia za Kenya na Djibouti.

Jeshi la Marekani lilipeleka askari 700 nchini Somalia kwa kisingizio cha kupambana na kundi lenye misimamo ya kufurutu ada la Al-Shabaab. Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon ilidai katika taarifa yake kwamba, wanajeshi hao waliopelekwa Somalia walikuwa wakitoa mafunzo kwa askari wa nchi hiyo ya kukabiliana na makundi ya Al Qaeda na Al-Shabaab.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

 

Donald Trump, ambaye hivi sasa anakamilisha siku zake za mwisho katika ikulu ya White House, mwezi  Desemba mwaka jana alichukua uamuzi wa kijeshi, wa kuamuru wanajeshi wa Marekani walioko Somalia wawe wameshaondoka katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita ifikapo mwanzoni mwa mwaka huu 2021.

Awali Rais Donald Trump aliitaka Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) sambamba na kuondoa nchini Somalia sehemu kubwa ya askari hao na kuwarejesha nyumbani, iunde kikosi kidogo kitakachobakia katika mji mkuu Mogadishu. Askari wa Marekani nchini Somalia wameondoka huku kukiwa kumebakia muda wa chini ya mwezi mmoja kabla ya nchi hiyo kuitisha uchaguzi mkuu.