Jan 19, 2021 03:14 UTC
  • Machafuko yaendelea Tunisia, jeshi kumiminwa mitaani kuwasaidia polisi

Vijana wenye hasira wameendelea kukaidi amri ya karantini ya nchi nzima huko Tunisia hasa nyakati za usiku na wameendelea kufanya maandamano licha ya kuweko maambukizi ya kirusi cha corona.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, waandamanaji wamemiminika katika mitaa ya Tunis, mji mkuu wa Tunisia na miji mingine kama Sousse, Kasserine, al Mahdia, al Monastir na miji mingine kadhaa na kupambana na polisi.

Baadhi ya vyombo vya habari vimesema kuwa, vijana hao wa Tunisia wanalalamika kutoona mabadiliko yoyote ya maana tangu baada ya kutokea mapinduzi ya wananchi miaka 10 iliyopita. Maandamano hayo aidha yanatokana na malalamiko ya vijana wa Tunisia wanaolalamikia matatizo ya kiuchumi na kijamii yanayotokana na kutokuweko utulivu wa kisiasa nchini humo ambao hivi karibuni ulilazimisha kubadilishwa Baraza la Mawaziri. Sababu nyingine ni matatizo mengi yaliyosababishwa na ugonjwa wa corona.

Jeshi la Tunisia mitaani

 

Askari wa kulinda usalama wametumia gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandanaji waliokuwa wakiwalenga kwa mawe askari hao, kufunga barabara na kuwasha moto majiani.

Huku hayo yakiripotiwa, wizara ya ulinzi ya Tunisia imesema kuwa, jeshi litatumwa katika miji ya nchi hiyo kwa ajili ya kuwasaidia polisi kukabiliana na vijana wanaofanya fujo hasa katika miji ya Siliana, Kasserine, Sousse na Bizerte.

Miji mingine iliyoshuhudia maandamano ya vijana hao Jumapili usiku ni pamoja na Kairuoa, Kebili, Nabeul na Manouba Gafsa. Wizara ya mambo ya ndani ya Tunisia imesema, karibu watu 1,000 wameshatiwa mbaroni hadi hivi sasa kwa kushiriki katika maandamano hayo ya fujo.

Tags