Jan 19, 2021 09:23 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia aionya Sudan, asema Addis Ababa si dhaifu

Waziri Mkuu wa Ethiopia ameionya Sudan na kusisitiza kwamba msimamo wa Addis Ababa mbele ya Khartoum si ishara ya udhaifu.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imemnukuu Abiy Ahmed akitoa onyo hilo na kuongeza kuwa, msimamo wetu mbele ya Sudan hauoneshi udhaifu, bali unaonesha nguvu zetu zilizochanganyika na subira na uvumilivu.

Matamshi hayo ya Waziri Mkuu wa Ethiopia yamekuja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Sudan Meja Jenerali Yasin Ibrahi Yasin kusema kuwa, Ethiopia hivi sasa inakusanya wanajeshi wake katika eneo la al Fushqa lenye mzozo baina ya Khartoum na Addis Ababa. Eneo hilo liko mashariki mwa Sudan.

Waziri Mkuu wa Sudan aliitaka Ethiopia iheshimu sheria za kimataifa za kuchunga mipaka ya nchi nyingine na ijifunze kuonesha ujirani mwema kwa kuondoa wanajeshi wake wote haraka iwezekanavyo katika maeneo ya Sudan.

Mpaka wa Ethiopia na Sudan

 

Ugomvi katika eneo la mapakani baina ya Sudan na Ethiopia umezidi kuwa mkubwa tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba 2020 wakati Ethiopia ilipoendesha operesheni za kijeshi za kuwang'oa waasi wa eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Vita hivyo vimepelekea zaidi ya wakimbizi 50 elfu wa Ethiopia wakimbilie mashariki mwa Sudan.

Ugomvi mkubwa uliopo baina ya Addis Ababa na Khartoum ni mashamba ya kilimo katika eneo la al Fushqa mkoani Qadarif mashariki mwa Sudan. Tangu takriban miaka 26 iliyopita, wanamgambo wa Ethiopia walilivamia eneo hilo, wakawafukuza wakulima wa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Sudan inaituhumu Ethiopia kuwa inawaunga mkono wanamgambo hao. Ethiopia imekasirishwa mno na uamuzi wa Sudan wa kuendesha operesheni za kuwafurusha wanamgambo hao katika eneo lake hilo.

Tags