Jan 19, 2021 11:41 UTC
  • Askari 2 wa UN wauawa CAR baada ya mahakama kuidhinisha ushindi wa Touadera

Genge la waasi limeua wanajeshi wawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA), masaa machache baada ya Mahakama ya Katiba kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa Disemba mwa uliopita, yaliyompa ushindi Faustin Archange Touadera.

Wanajeshi hao wa MINUSMA, mmoja raia wa Gabon na mwengine wa Morocco waliuawa jana Jumatatu baada ya msafara wa magari yao ya deraya kuviziwa na kushambuliwa na waasi katika mji wa Bangassou ulioko kusini mwa nchi.

Shambulio hilo ni katika mfufulizo wa hujuma na utekaji nyara uliofanywa katika siku za hivi karibuni na magenge ya waasi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mankeur Ndiaye, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kikosi cha MINUSMA 'kimelipa gharama kubwa' lakini hakitasalimu amri, bali kitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia na mchakato wa uchaguzi.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya askari mwingine wa Umoja wa Mataifa kutoka Burundi kuuawa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Rais Touadera aliyeshinda muhula wa pili

Hii ni katika hali ambayo, MINUSCA ilitangaza mwishoni mwa wiki kuwa imeudhibiti tena mji huo wa Bangassou wenye utajiri wa madini ya almasi, ulioko umbali wa Kilomita 750 kutoka mji mkuu Bangui, uliokuwa umetekwa na waasi.

Mapema jana, Daniele Darlam, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Katiba wa CAR kwa niaba ya majaji wenzake aliidhinisha ushindi wa Toudera katika uchaguzi wa rais wa Disemba 27. Touadera ameshinda muhula wa pili kwa kuzoa asilimia 53.1 ya kura, na kumbwaga Waziri Mkuu wa zamani, Anicet Georges aliyeambulia asilimia 21.6. 

Tags