Jan 19, 2021 11:57 UTC
  • Mkuu wa UN ataka askari ajinabi waondoke Libya haraka iwezekavyo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka wanajeshi na mamluki wote wa nchi ajinabi waondoke nchini Libya haraka iwezekanavyo.

Antonio Guterres alitoa mwito huo jana Jumatatu katika ripoti aliyoiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo pia imepongeza hatua za maana zilizopigwa ndani ya miezi michache iliyopita za kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Amesema mazungumzo ya kimataifa yanayosimamiwa na UN juu ya mustakabali wa kisiasa na kiusalama ya Libya yamezaa matunda, na hivi sasa nchi hiyo ipo katika mkondo wa kurejea katika amani, ustawi na uthabiti.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa wadau wote wa kieneo na kimataifa kuheshimu vipengee vya makubaliano ya kusitisha vita yaliyopasishwa Oktoba 23 mwaka jana.

Libya iliyogawanyika vipande vipande

Moja ya vipengee hivyo ni kuondoka askari ajinabi nchini Libya katika kipindi cha miezi mitatu, muhula ambao unamalizika siku chache zijazo, yaani Januari 23. 

Kwa sasa Libya ina serikali mbili; moja ikiwa ile inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa yenye makao makuu huko Tripoli, mji mkuu wa Libya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj, na serikali nyingine ina makao yake katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi hiyo. Serikali ya Tobruk inaungwa mkono na Imarati, Misri, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ulaya. Uturuki inaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.

Tags