Jan 20, 2021 07:50 UTC
  • UNHCR: Wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaoingia Cameroon wanaongezeka

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, idadi ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaokimbia makazi yao na kuelekea Cameroon inazidi kuongezeka.

Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa, watu zaidi ya 5,000 wameyahama makazi yao hivi karibuni wakikimbia mashambulizi ya waasi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati hasa kwenye mji wa Magharibi wa Bouar na kuingia nchi jirani ya Cameroon kusaka usalama.

Katika makazi ya wakimbizi ya Garoua Boulai nchini Cameroon, maelfu ya watu wamewasili hivi karibuni kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wengi wakiwa wanawake na watoto na wamekusanyika wakisubiri kusajiliwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa UNHCR kuna kila ishara kwamba makundi yenye silaha yatashambulia katika sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Afrika ya Kati na ingawa mipaka baina ya CAR, Cameroon na Chad imefungwa asasi hiyo ya Umoja wa Mataifa inaendelea kuzisihi nchi hizo kuifungua ili wanaokimbia kwenda kusaka usalama waweze kunusuru maisha yao.

Rais Faustin-Archange Touadéra

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imepasisha ushindi wa Rais Faustin-Archange Touadéra kufuatia uchaguzi uliofanyika tarehe 27 Desemba mwaka jana.

Touadera alishinda muhula wa pili kwa kuzoa asilimia 53.1 ya kura, na kumbwaga Waziri Mkuu wa zamani, Anicet Georges aliyeambulia asilimia 21.6, katika uchaguzi ambao ulikabiliwa na changamoto na vitisho kutoka kwa makundi ya wabeba silaha.