Jan 20, 2021 07:51 UTC
  • Mhubiri wa Kikristo: Vyombo vya habari havimzungumzii Sheikh Zakzaky kwa kuiogopa serikali

Mhubiri mmoja wa Kikristo nchini Nigeria amevikosoa vyombo vya habari vya nchi hiyo kwa kufumbia macho dhulma iliyofanywa dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na wafuasi wake.

Roland Sanda amesema vyombo vya habari vya Nigeria kutokana na kuogopa vitisho vya serikali ya Rais Muhamadu Buhari, vimeamua kunyamazia kimya kadhia nzima ya Sheikh Zakzaky.

Aidha amesema, inaonekana kuwa, serikali ya Nigeria inataka watu wanyamazie kimya kabisa matukio yanayohusiana na Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na harakati yake ya Kiislamu.

Mhubiri huyo wa Kikristo amesema, hata mashinikizo na juhudi za asasi za haki za binadamu hazijazaa matunda kutokana na serikali ya Buhari kutokuwa tayari kusikiliza vilio hivyo.

Aidha kiongozi huyo wa Kikristo amemsifu Sheikh Ibrahim Zakzaky na kumtaja kuwa mtu anayepigania amani.

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe

 

Roland Sanda kadhalika amesema kuwa, Sheikh Zakzaky na wafuasi wake wamedhulumiwa sana kwani yote yaliyofanywa dhidi yao yalifanyika pasina ya kuthibiti makossa.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake walikamatwa na vyombo vya dola vya Nigeria tarehe 13 Disemba mwaka 2015 katika shambulizi lililofanywa na askari wa nchi hiyo dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyyatullah katika mji wa Zaria. 

Siku hiyo jeshi la Nigeria liliwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa katika kituo hicho cha kidini na nyumba na msomi huyo na kuua shahidi mamia ya watu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky.