Jan 20, 2021 07:52 UTC
  • Ismail Haniya autaka Umma wa Kiislamu uwe kitu kimoja katika kuiunga mkono Palestina

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, Umma wa Kiislamu unapaswa kuandaa mipango na mikakati jumuishi katika kuliunga mkono taifa la Palestina na muqawama kama njia ya kukabiliana na njama na hatari zinazoikabili kadhia ya Palestina.

Ismail Haniya amepongeza na kuthamini himaya na uungaji mkono wa nchi zilizoshiriki katika mkutano kwa njia ya mawasiliano ya Intaneti wa Wakuu wa Kamisheni za Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni za Mabunge ya Nchi Zinazoiunga Mkono Palestina na kueleza kwamba, kufanyika mkutano huu katika anga ya migawanyiko na hitilafu zinazoshuhudiwa katika eneo la Asia Magharibi ni ishara ya wazi kwamba, Palestina ni kadhia moja na jumuishi ambayo inapewa umuhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amebainisha kwamba, Umma wa Kiislamu licha ya hitilafu zilizopo baina yao, lakini una mtazamo mmoja kuhusiana na kadhia ya Baitul-Muqaddas, Palestina na muqawama na kusimama kidete dhidi ya mipango ya Uzayuni na ubeberu wa Marekani katika eneo.

Masjidul-Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu

 

Aidha amesema: Tuna haja ya kufikia utendaji na mkakati jumuishi ambao msingi wake utakuwa ni umoja wa taifa la Palestina, kushikamana na misingi ya kitaifa, kutofumbia macho ardhi za Palestina na kutomtambua rasmi adui Mzayuni.

Kadhalika Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, mapambano na muqawama ndio chaguo pekee la kuwatimua Wazayuni wavamizi kutoka katika ardhi za Palestina wanazozikalia kwa mabavu.