Jan 20, 2021 07:53 UTC
  • Marekani yatangaza vikwazo dhidi ya maafisa wa serikali ya Tanzania waliovuruga uchaguzi

Serikali ya Marekani imetangaza vikwazo vya kuingia nchini humo maafisa wa juu wa serikali ya Tanzania, wanaotuhumiwa kuhujumu uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka uliopita na kumuwezesha rais John Pombe Magufuli kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 80.

Uamuzi huo umetangazwa na Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani anayemaliza muda wake, ambaye amesema katika taarifa yake hiyo kwamba, waliolengwa ni wale walioharibu mchakato wa demokrasia na kukiuka haki za binadamu nchini Tanzania. Hata hivyo, serikali ya Marekani haijaweka wazi majina ya maafisa hao ambao imewazuia kuingia nchini Marekani.

Pompeo amesema kulikuwa na vitisho vingi na kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani, pamoja na kuripotiwa visa vya udanganyifu katika uchaguzi huo na kuzimwa kwa mtandao, hatua ambazo ziliufanya uchaguzi huo kutokuwa huru na haki.

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani anayemaliza muda wake

 

Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania na  Serikali kupitia Waziri wake wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi ilieleza kwamba uchaguzi huo huru na wa haki.

Dakta John Pombe Magufuli aliibuka mshindi wa kinyang'anyiro cha urais cha Oktoba 28 mwaka jana, baada ya kupata kura zaidi ya milioni 12, sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali zilizopigwa, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Tundu Lissu, mgombea wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyepata kura karibu milioni 2 alipinga matokeo ya uchaguzi huo, akisisitiza kuwa zoezi hilo liligubikwa na mizengwe na uchakachuaji wa matokeo.