Jan 21, 2021 04:34 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe aaga dunia kwa corona

Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Sibusiso Moyo ameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Serikali ya Harare imethibitisha habari za kuaga dunia Moyo akiwa na umri wa miaka 61. Waziri huyo ameingia katika orodha ya mawaziri na maafisa wa ngazi za juu wa Zimbabwe walioaga dunia kutokana na virusi vya corona.

Jenerali huyo wa zamani wa Zimbabwe aligonga vichwa vya habari mwaka 2017, alipotangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limetwaa madaraka, hatua iliyomlazimisha rais wa wakati huo wa nchi hiyo, hayati Robert Mugabe aachie ngazi.

Wiki iliyopita, Ellen Gwaradzimbe, Waziri wa Masuala ya Mkoa wa Manicaland nchini Zimbabwe alifariki dunia kwa corona, miezi michache baada ya Perrance Shiri, aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Kilimo wa nchi hiyo kuaga dunia kwa maradhi hayo hayo ya kuambukiza.

 

Zimbabwe chini ya karantini hadi Januari 31

Mapema mwezi huu, serikali ya Zimbabwe ilitangaza kuwa sheria ya karantini ya nchi nzima imeanza kutekelezwa nchini humo kwa mara nyingine tena kutokana na kuongezeka maambukizi mapya ya corona. Sheria hiyo inatekelezwa baina ya Januari 5 hadi Januari 31.

Takwimu rasmi za karibuni zilizotangazwa na Wizara ya Afya ya Zimbabwe zinaonyesha kuwa, tangu kuenea maambukizi ya corona nchini humo hadi sasa watu 28,675 wameripotiwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 huku wengine 825 wakiaga dunia kwa ugonjwa huo. Kadhalika watu zaidi ya 15 elfu waliokuwa wameambukizwa maradhi hayo nchini humo wamepata afueni.

Tags