Jan 21, 2021 11:53 UTC
  • Misri yakaribisha mapatano ya Libya kuhusu mchakato wa katiba ya nchi hiyo

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imekaribisha mapatano yaliyofikiwa na pande za Libya kuhusu mchakato wa katiba ya nchi hiyo.

Katika taarifa iliyotoa siku ya Jumatano Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeunga mkono mapatano yaliyofikiwa na pande za Libya katika mji wa Hurghada Misri kuhusu mchakato wa katiba ya nchi hiyo chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. 

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeongeza kuwa, Cairo inaunga mkono jitihada zilizopelekea kufikiwa mapatano kuhusu suala la kuendesha kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba ya Libya kwa ajili ya kujiandaa kuendesha uchaguzi mkuu huko Libya tarehe 24 mwezi Disemba mwaka huu. 

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imebainisha kuwa, nchi hiyo inasubiri kuwa mwenyeji wa duru ya tatu na ya mwisho ya mchakato wa katiba ya Libya mnamo mwezi ujao wa Februari itakayohudhuriwa pia na Kamishma Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Libya kwa lengo la kuandaa ramani ya njia kwa ajili ya kuendesha kura ya maoni na uchaguzi nchini humo.   

Duru za habari pia zimearifu kuhusu kufikiwa mapatano kati ya wajumbe wa kamati ya katiba ya Libya kwa ajili ya kuendesha kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi hiyo.  

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Libya ina serikali mbili moja ikiwa na makao yake mashariki na nyingine magharibi mwa nchi baada ya kung'olewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo Kanali Muammar Qaddafi. Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Libya ina makao yake katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli huku ikiungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar kwa jina la Jeshi la Kitaifa la Libya pia wanaiunga mkono serikali yenye makao yake mashariki mwa nchi.  

Jenerali muasi, Khalifa Haftar 

 

Tags