Jan 22, 2021 08:19 UTC
  • Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza aizuru Sudan baada ya zaidi ya muongo mmoja

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza ameitembelea Sudan katika safari iliyotajwa kuwa ya aina yake kwa afisa huyo wa ngazi za juu wa nchi hiyo ya Ulaya ikiwa imepita zaidi ya muongo mmoja.

Akiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum hapo jana, Dominic Raab amekutana na kufanya mazungumzo na Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, Kiongozi wa Baraza la Utawala, Waziri Mkuu Abdalla Hamdok na Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni  wa Sudan Omar Qamar al-Din.

Duru za karibu zinaeleza kuwa, miongoni mwa ajenda za mazungumzo ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza na vingozi wa Sudan ni uhusiano wa pande mbili, hali ya mambo katika mpaka wa Sudan na Ethiopia na mzozo wa Bwawa la al-Nahdha baina ya Sudan, Ethiopia na Misri ambao unatishia kuibuka mgogoro wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo.

Dominic Raab, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza akiwa katika mazungumzo na Abdul-Fattah al-Burhan, Kiongozi wa Baraza la Utawala nchini Sudan (21.01.2021)

 

Katika hatua inayolenga kupiga jeki mageuzi ya kiuchumi yanayofanywa na serikali ya Khartoum, Dominic Raab ametangaza kuwa, nchi yake itaipatia Sudan msaada wa pauni 40/-milioni kwa ajili ya kusaidia watu milioni 1.6 wa nchi hiyo ya Kiafrika wanaohitajia msaada wa moja kwa kwa moja wa fedha.

Kabla ya kuelekea Sudan, siku ya Jumatano Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza aliitembelea Kenya ambako alisema kuwa, London itaipatia serikali ya Nairobi msaada wa fedha ili iweze kukabiliana na changamozo mbalimbali zinazoikabili kama mabadiliko ya tabianchi, vita dhidi ya harakati za misimamo ya kufurtu mipka na ufanikishaji wa chanjo ya corona.

Tags