Jan 22, 2021 08:19 UTC
  • Baada ya mawaziri kadhaa kuaga dunia kwa Corona; Zimbabwe yatangaza maombi ya kitaifa

Zimbabwe imetangaza siku tatu za ibada na maombi ya kitaifa ili kumuomba Mwenyezi Mungu alinusuru taifa hilo na janga la Corona ambalo hadi sasa limechukua roho za mawaziri kadhaa wa nchi hiyo.

Maombi hayo ya siku tatu yanaongozwa na mke wa Rais wa nchi hiyo Mama Auxillia Mnangagwa.

Mke huyo wa Rais  Emmerson Mnangagwa amewaomba wanawake wote wa Zimbabwe na walio nje ya nchi hiyo kuungana naye katika maombi hayo akisema “Tunahitaji kufanya mkakati madhubuti kuanzia nyumbani, kunawa mikono, kuvaa barakoa sahihi na cha msingi zaidi kila mmoja azingatie kanuni za afya na kuwa salama kwa kuepuka misongamano.”

Hayo yanajiri katika hali ambayo, juzi Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Zimbabwe, Sibusiso Moyo aliaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19.

Jenerali huyo wa zamani wa Zimbabwe aligonga vichwa vya habari mwaka 2017, alipotangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limetwaa madaraka, hatua iliyomlazimisha rais wa wakati huo wa nchi hiyo, Robert Mugabe aachie ngazi.

Sibusiso Moyo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Zimbabwe aliyefariki dunia kwa corona

 

Wiki iliyopita, Ellen Gwaradzimbe, Waziri wa Masuala ya Mkoa wa Manicaland nchini Zimbabwe alifariki dunia kwa corona, miezi michache baada ya Perrance Shiri, aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Kilimo wa nchi hiyo kuaga dunia kwa maradhi hayo hayo ya kuambukiza.

Mapema mwezi huu, serikali ya Zimbabwe ilitangaza kuwa sheria ya karantini ya nchi nzima imeanza kutekelezwa nchini humo kwa mara nyingine tena kutokana na kuongezeka maambukizi mapya ya corona.

Tangu kuenea maambukizi ya corona nchini Zimbabwe hadi sasa watu 30,047 wameripotiwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 huku wengine 917 wakiaga dunia kwa ugonjwa huo.