Jan 22, 2021 11:53 UTC
  • Umoja wa Mataifa watangaza tarehe ya uchaguzi wa Serikali ya Mpito Libya

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umetangaza kuwa, wagombea wa nafasi za uongozi katika serikali mpya ya mpito ya Libya wanatakiwa wajulikane katika kipindi cha wiki moja ijayo ili mwanzoni mwa mwezi ujao wa Februari kupigwe kura ya kuwachagua wagombea hao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sada al Balad, mwezi Novemba 2020 Umoja wa Mataifa uliainisha wajumbe 75 wa Baraza la Mazungumzo ya Kisiasa la Libya huko Tunis, mji mkuu wa Tunisia ili waweze kufanya kazi ya kuandaa muongozo wa uchaguzi wa nchi nzima ya Libya. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 24 Disemba mwaka huu wa 2021.

Baada ya kupita wiki kadhaa za majadiliano, wajumbe wa baraza hilo hivi karibuni walifikia mapatano kuhusu mchakato wa kuchagua Baraza Kuu jipya litakaloundwa na watu watatu na Waziri Mkuu mmoja kwa ajili ya kuendesha serikali ya kipindi cha mpito.

Umoja wa Mataifa umesema, wajumbe wa Baraza la Mazungumzo ya Kisiasa la Libya watapiga kura tarehe Mosi hadi 5 mwezi ujao wa Februari ili kuchagua viongozi wa serikali hiyo ya mpito.

Mafahali wawili wakuu katika mgogoro wa Libya. Fayez al Sarraj (kushoto) na jenerali muasi Khalifa Haftar

 

Baada ya kufikiwa hatua hiyo, Fayez al Sarraj, Mkuu wa Baraza la Uongozi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya amemtumia ujumbe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo akiutaka uendelee kuunga mkono jitihada za kuitishwa uchaguzi mkuu wa Rais na Bunge katika kona zote za Libya tarehe 24 Disemba, 2021.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Libya ina serikali mbili moja ina makao yake mashariki na nyingine magharibi mwa nchi hiyo. Mzozo mkubwa umezuka nchini Libya kwa takriban miaka 10 sasa na nchi hiyo haijawahi kushuhudia utulivu wa maana wa angalau siku moja katika kipindi chote hicho.

Tags