Jan 23, 2021 05:06 UTC
  • Iran kuanzisha kituo kikubwa zaidi cha Teknolojia nchini Kenya

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuanzisha kituo kikubwa cha ubunifu na teknolojia katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi ikiwa ni katika mkakati wa kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili rafiki.

Balozi wa Iran nchini Kenya, Ja’afar Barmaki amesema ‘Kituo cha Iran cha Ubunifu na Teknolojia (IHIT), kitazinduliwa wiki ijayo katika eneo la Kilimani mjini Nairobi. Akifafanua zaidi kuhusu kituo hicho, Balozi Barmaki amesema: “Kituo hiki ni cha kwanza cha aina yake barani Afrika na ni kituo kikubwa zaidi cha Iran duniani ambacho kimeanzishwa kwa lengo la kuwapa wengine teknolojia yake ambayo imeweza kuipata katika miaka ya hivi karibuni.”

Hali kadhalika amedokeza kuwa wiki ijayo, wawakilishi wa mashirika 40 ya kiteknolojia ya Iran katika nyuga za petrokemikali, nishati jadidika, utegenezaji dawa, bioteknolojia na nanoteknolojia watatembelea Kenya.

Ujumbe huo utaongozwa na Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia sayansi na teknolojia Dakta Sorena Sattari ambaye atakutana na wafanyabiashara katika sekta ya teknolojia nchini Kenya ili kujadili njia za kuimarisha uhusiano baina ya nchi mbili.

Balozi Barmaki amesema katika sera zake za kigeni, Iran inaitazama Kenya kama nchi rafiki yenye miundomsingi bora na iliyostawi na hivyo imeamua kuanzisha kituo hicho kikubwa cha mabadilishano ya teknolojia mjini Nairobi. Aidha amesema Iran inaweza kutumia nafasi ya kistratijia ya Kenya kuweza kuingia katika nchi zingine za eneo.

Iran na Kenya zina uhusiano wa kirafiki na zinashirikiana katika sekta za biashara, utamaduni, siasa n.k.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imelipa kipaumbele suala la mashirika ambayo msingi wake ni elimu yaani knowledge-based na hivi sasa kuna mashirika zaidi ya 5,000 ya aina hiyo ambayo yanajishughulisha katika uga wa teknolojia ya kisasa nchini.

Wafanyabiashara na wadau wa sekta ya teknolojia nchini Kenya ambao wanataka kushiriki katika kikao na wawakilishi wa mashirika ya Iran katika kikao kitakachofanyika Januari 27 katika kituo hicho cha ubunifu na teknolojia wanaweza kutembelea tovuti ifuatayo kwa maelezo zaidi  http://b2b.ihit.co.ke/registration

 

Tags