Jan 23, 2021 11:52 UTC
  • Maiti 139 zagunduliwa katika makaburi ya umati Libya

Jumla ya maiti 139 zimegunduliwa katika makaburi ya umati katika mji wa Tarhauna, magharibi mwa Libya tokea mwezi Juni mwaka uliopita 2020 hadi sasa.

Hii ni baada ya miili mingine ya watu 16 kugunduliwa katika makaburi ya umati huko magharibi mwa Libya hivi karibuni. Familia za wahanga hao jana Ijumaa ziliiswalia miili hiyo iliyogunduliwa mkoani Tarhauna.

Lutfi Tawfeeq, Mkuu wa Idara ya Kutafuta Maiti amesema miili hiyo ilibainika baada ya kufukiliwa makaburi 47 ya umati mkoani Tahrauna, yapata kilomita 90 kusini mwa mji mkuu Tripoli.

Mji wa Tarhauna ulikuwa ngome ya vikosi vya Jenerali muasi Khalifa Haftar wakati wa kampeni zao za kutaka kuiteka Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Jenerali Khalifa Haftar

Wanajeshi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya yenye makao yake Tripoli  mwaka jana walifanikiwa kuchukua udhibiti wa mji huo baada ya kuwatimua wanamgambo wa Haftar wanaopata himaya ya Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudia na baadhi ya nchi za Magharibi.

Huko nyuma, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alieleza kushtushwa kwake kutokana na kugunduliwa makaburi hayo ya umati nchini Libya katika eneo hilo ambalo lilikuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa wakioongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar.

Tags