Jan 25, 2021 07:39 UTC
  • Polisi Sudan wakabiliana na waandamanaji wanaolalamikia ughali wa maisha

Polisi nchini Sudan wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa na hasira katika mji mkuu Khartoum ambao walikuwa wanalalamikia ugali wa maisha.

Waandamanaji hao walikusanyika katika barabara kuu ya upande wa mashariki mwa Khartoum ambapo waliweka vizuizi barabarani na kuchoma matairi kama njia ya kubainisha hasira zao kufuatia ongezeko kubwa la ughali wa maisha, uhaba wa chakula na kukatika umeme mara kwa mara.

Aidha maandamano yamefanyika katika mji wa Omdurman karibu na Khartoum ambapo waandamanaji pia wameweka vizuizi barabarani kulalamikia ugali wa maisha.

Sudan ilitumbukia katika mgogoro wa kiuchumi kabla na baada ya kupinduliwa dikteta Omar al Bashir Aprili 2019. Bashir alipinduliwa na jeshi baada ya maandamano ya miezi kadhaa ya wananchi ambao walikuwa wanalalmikia nyongeza ya bei za bidhaa muhimu.

Maandamano ya wananchi wa Sudan kupinga mapatano baina ya nchi yao na utawala haramu wa Israel

Hivi sasa pia kutokana na janga la COVID-19, Sudan yenye idadi ya watu milioni 40, inakumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Wananchi wanalazimika kupanga foleni masaa kadhaa kununua mkate huku kukiwa na uhaba mkubwa wa umeme. Ughali wa maisha ulifika asilimi 269 mwezi jana huku nchi hiyo ikiwa na deni la zaidi ya dola bilioni 60.

Hayo yanajiri wakati ambao Septemba mwaka jana, utawala wa mpito nchini Sudan ulitangaza kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel kwa matarajio ya kupata misaada ya kifedha ya Marekani. Hata hivyo hali ya kiuchumi imezidi kuwa mbaya na wananchi pia wameandamana mara kadhaa kupinga uamuzi wa nchi yao kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.

 

 

Tags