Jan 25, 2021 09:38 UTC
  • Kuendelea machafuko nchini Tunisia

Licha ya kupita takriban muongo mzima tangu yalipotokea mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na kuchochea mapinduzi mengine katika nchi kadhaa za ulimwengu wa Kiarabu, lakini bado wananchi wa nchi hiyo wanalalamikia matatizo mengi ya kijamii na kisiasa nchini mwao.

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita na licha ya kuweko karantini ya corona na kutoruhusiwa magari na watu kutembea ovyo barabarani, lakini maandamano yanaendelea kufanyika nyakati za usiku katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis na baadhi ya miji muhimu ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Ijapokuwa mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011 huko Tunisia yalikuwa ni mabadiliko makubwa ya kisiasa na kulipatikana matumaini makubwa ya kufanyika marekebisho ya kiuchumi na kijamii nchini humo, lakini karibu miaka 10 sasa imepita na hakuna mabadiliko yoyote ya maana waliyoyashuhudia wananchi. Sehemu kubwa ya wananchi wa Tunisia wameendelea kuwa na hali mbaya si ya kiuchumi tu, lakini pia ya kisiasa na kijamii hususan kiwango kikubwa cha ukosefu wa kazi kati ya vijana, umaskini, mfumuko wa bei na kadhalika. Hali hiyo imezidi kuwa mbaya baada ya kuzuka ugonjwa wa COVID-19 na kuanza kuchukuliwa hatua kali za kukabiliana na ugonjwa huo wa kuambukiza ambao hadi leo hii hauna dawa. Sasa hivi sehemu kubwa ya wanaoandamana wana wasiwasi na kupotea malengo ya mapinduzi yao ya mwaka 2011 na kurejea katika enzi za dikteta Zine al-Abidine Ben Ali. 

Zine al-Abidine Ben Ali

Dikteta  Zine al-Abidine Ben Ali

 

Maher Obaid, mmoja wa waandamanaji wenye hasira amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akilalamika kwamba, mgogoro wa ukosefu wa kazi na hali mbaya ya kimaisha imetulazimisha turudi tena mitaani kwa ajili ya kupigania haki zetu kutoka kwa viongozi mafisadi waliotumia vibaya fursa ya mapinduzi ya wananchi. Watu kama mwananchi huyo wa Tunisia ni wengi sana. Hao ni wale wale wananchi ambao walimpindua dikteta Zine al-Abidine Ben Ali, na sasa wameamua kumiminika tena mitaani katika masaa ya mwisho ya usiku kuilaani serikali na utendaji wake.

Hali ya malalamiko nchini Tunisia ni mbaya kiasi kwamba hivi karibuni, Rached al Ghannouchi, Spika wa Bunge la Wananchi wa Tunisia aliwataka wananchi, vyama na taasisi zote za kisiasa kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kuikoa nchi hiyo. Aliwatumia ujumbe waandamanaji akiwaambia kwamba anaelewa vizuri mateso na matatizo makubwa ya maeneo maskini na shida za vijana wasio na kazi. 

Kuongezeka ufisadi na mwanya wa kitabaka kati ya wananchi na viongozi ni jambo jingine lililowakasirisha sana wananchi wa Tunisia. Ijapkuwa sehemu kubwa ya ufisadi wa kifedha na kiidara ni matatizo sugu na ya muda mrefu yaliyorithiwa nchini Tunisia tangu enzi za utawala wa kidikteta, lakini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni si tu hakuna hatua zozote za maana zilizochukuliwa kwa ajili ya kukabiliana na matatizo hayo, bali pia hali ya kijamii na kisiasa imezidi kuchochea ufisadi na tofauti za kimatabaka nchini humo.

Rached al Ghannouchi, Spika wa Bunge la Wananchi wa Tunisia

 

Issam al Chebbi, Katibu Mkuu wa chama cha Jamhuri cha Tunisia anasema: Mapinduzi nchini humo yamepata ushindi lakini kuna wajibu wa kuangaliwa upya njia za kugawa kiuadilifua utajiri wa nchi hiyo.

Amma suala jingine lililochochea maandamano ya wananchi wenye hasira huko Tunisia, ni kuongezeka ukandamizaji wa polisi kwa wapinzani wa serikali. Katika kukabiliana na waandamanaji, polisi wa Tunisia wanatumia nguvu na mabomu ya kutoa machozi suala ambalo limezidisha hasira za wananchi. Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limelalamikia vipigo na mateso wanayofanyiwa watu wanaokamatwa na polisi katika maandamano hayo. Shirika hilo limesambaza picha ya watu hao na kusema kwamba waandamanaji wengi wametiwa mbaroni. Hadi hivi sasa karibu waandamanaji 630 wameshatiwa mbaroni huko Tunisia na hiyo ni kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Vitendo hivyo vimechochea zaidi maandamano ya kupinga serikali katika mji mkuu Tunis na miji mingine muhimu huku waandamanaji wakipiga nara wakisema, hatukubali kurejea katika utawala wa zamani wa kipolisi.

Tags