Jan 25, 2021 23:39 UTC
  • Serikali ya Tanzania yaafiki kuwarejesha kwao mamia ya wafungwa wa Ethiopia

Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia kuwarejesha kwao wafungwa 1,789 raia wa Ethiopia walioko kwenye magereza mbalimbali ya nchi hiyo wakituhumiwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria.

Serikali ya Tanzania imeitaka Ethiopia kufanya taratibu za kuwarejesha nyumbani wafungwa hao ili wakatumikie na kujenga taifa lao.

Uamuzi huo umefikiwa katika mazungumzo ya kuhitimisha ziara ya siku moja ya rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde wa Ethiopia ambaye jana alitembelea Tanzania.

Baada ya Bi Sahle Zewde kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Chato alipokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli ambapo Marais hao walifanya mazungumzo ya ana kwa ana katika ikulu ya Chato kwa takribani saa tatu kabla ya kujitokeza tena hadharani.

Rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopia akikagua gwaride na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli

 

Aidha matunda mengine ya safari ya Rais wa Ethiopia hapo jana nchini Tanzania ni pande mbili kuazimia kushirikiana kwenye biashara ya wanyama na mazao yatokanayo na wanyama; kwani Ethiopia imepiga hatua zaidi katika sekta hiyo, hivyo Tanzania itajifunza na kuweza kunufaika katika ushirikiano huo.

Rais wa Ethiopia amewaambia waandishi wa habari kwamba, wamekubaliana pia na Rais Magufuli kuwa Kiswahili kianze kufundishwa katika Chuo Kikuu cha Adis Ababa huko Ethiopia. Aidha Rais Zewde alisema kuwa, maneno ya kwanza ya Kiswahili aliyojifunza ni “Acha kelele mtoto amelala”.

Tanzania na Ethiopia zimekuwa na uhusiano wa kihistoria na katika kudumisha uhusiano huo Ethiopia imeahidi kuipatia tena Tanzania eneo la kujenga ubalozi wake baada ya eneo la awali kuchuliwa na serikali kutokana na kutokuendelezwa na serikali ya Tanzania.