Jan 25, 2021 23:40 UTC
  • Waandamanaji waliokuwa wakipinga kusikilizwa kesi ya Sheikh Zakzaky washambuliwa na vikosi vya usalama

Vikosi vya usalama nchini Nigeria vimevamia maandamano ya wananchi ya kupinga kusikilizwa kesi ya Sheikh Iibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Ripoti kutoka Nigeria zinasema, vikosi vya usalama jana vilivamia maandamano ya wananchi na kutumia mkono wa chuma kuwatawanya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky waliokuwa wakiandamana kupinga jinsi mchakato wa kusikilizwa kesi ya kiongozi wao unavyoendeshwa.

Ripoti zaidi zinaeleza kuwa, miji mbalimbali ya Nigeria jana ilishuhudia maandamano ya wananchi wanaolalamika kutopokea moja kwa moja habari zinazohusiana na kesi ya Sheikkh Zakzaky.

Kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ambayo ilianza kusikilizwa tangu Novemba mwaka jana bila ya yeye kuhudhuria mahakamani, iliendelea tena jana kwa mahakama kusikiliza upande wa mashahidi.  Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo Jumanne.

Maandamano ya wananchi wa Nigeria ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

 

Wafuasi wa Sheikh Zakzaky wamekuwa wakivitaka vyombo vya usalama vimuachilie huru kiongozi huyo pamoja na mkewe kwani hawana hatia yoyote kwa mujibu wa amri ya iliyowahji kutolewa huko nyuma na mahakama.

Wakati huo huo, mke wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Malama Zeenat ambaye alikuwa akishikiliwa kizuizini pamoja na mumewe amehamishiwa hospitali kwa amri ya mahakama baada ya kuambukizwa virusi vya Corona.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake walikamatwa na vyombo vya dola vya Nigeria tarehe 13 Disemba mwaka 2015 katika shambulizi lililofanywa na askari wa nchi hiyo dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyyatullah katika mji wa Zaria.