Feb 13, 2021 04:50 UTC
  • UNICEF: Watoto wanateseka katike eneo lenye mgogoro la Tigray, Ethiopia

Kadri misaada ya dharura na wafanyakazi wa kusambaza misaada hiyo wanafikia eneo la mzozo la Tigray huko Ethiopia, taswira halisi ya masikitiko inazidi kuibuka jinsi watoto kwenye eneo hilo wanavyoendelea kuteseka.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema, idadi kubwa ya familia zimetenganishwa wakati wa kukimbia mapigano na miongoni mwa wakimbizi wa ndani ni watoto ambao wamekimbia wenyewe bila mzazi au mlezi.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa Ijumaa Addis Ababa Ethiopia, Nairobi Kenya, Geneva Uswisi na New York Marekani imesema kuwa kati ya tarehe 4 na 7 mwezi huu wa Februari, timu ya shirika hilo ilifika katika mji wa Shire katikati ya Tigray ikiwa na malori 6 yaliyosheheni misaada ya dharura, ikiwa ni shehena ya kwanza tangu mapigano yaanze Tigray tarehe 4 mwezi Novemba mwaka jana.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, “Mji huo ni makazi ya watu 170,000 lakini sasa una takribani wakimbizi wa ndani 52,000 na wengine wengi wameendelea kuwasili.”

Hadi mwisho wa mwezi Januari, UNICEF kwa ushirikiano na serikali ya Ethiopia na wadau huko Tigray na maeneo jirani imeshachukua hatua kadhaa za dharura ikiwemo kupima zaidi ya watoto 450,000 wenye  umri wa chini ya miaka 5 kama wana utapiamlo na kuwapatia huduma za kuokoa maisha kwa wale waliobainika kuwa na utapiamlo.

Hali kadhalika imefikishia watu 137,000 wakiwemo wakimbizi wa ndani na wenyeji huduma za maji safi na salama. Hali kadhalika wasichana barubaru na wanawake 5,400 wamepatiwa vifaa vya kujisafisha.

Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia limekuwa likishuhdia mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya waasi wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF.

Mbali na maelfu ya raia kuuawa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Tags