Feb 14, 2021 03:45 UTC
  • UN yataka mashirika ya misaada yapewe uhuru wa kuingia Tigray, Ethiopia

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka serikali ya Ethiopia iruhusu mashirika ya misaada kuingia na kufanya kazi zake kwa uhuru katika eneo la Tigray ili kuokoa roho za wakazi wa eneo hilo.

Stephen Dujarric amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema hayo na kuongeza kuwa, maafisa wa mashirika ya misaada wamesema kwamba, baada ya serikali ya Ethiopia kuafiki kuingia katika eneo la Tigray wafanyakazi 53 wa misaada ya kibindamu, sasa hivi mashirika ya Umoja wa Mataifa yako mbioni kutuma watu hao, hata hivyo amesema hawatoshi.

Eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia hivi karibuni lilikumbwa na mapigano makali baina ya jeshi la serikali na Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (TPLF).

Wanamgambo wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (TPLF)

 

Serikali ya Ethiopia inaituhumu harakati hiyo kuwa inafanya njama za kujitenga. Hivi karibuni Addis Ababa ilitangaza kuwa jeshi la serikali limeudhibiti kikamilifu mji wa Mek'ele, makao makuu ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo. 

Habari kutoka eneo hilo zinasema kuwa, kumefanyika mauaji mengi ya kiholela dhidi ya raia na watu wa kawaida wakati wa mapigano baina ya jeshi la serikali na wapiganaji wa harakati hiyo ya ukombozi wa wananchi wa Tigray.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wameuawa na zaidi ya laki 9 na 50 elfu wamelazimika kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethioia huku 50,000 kati yao wakikimbilia katika nchi jirani ya Sudan. 

Tags