Feb 17, 2021 02:24 UTC
  • Kuanza kikao cha kundi la nchi 5 za Sahel Afrika huko Chad

Kikao cha kundi la nchi 5 za Sahel Afrika kimeanza katika mji mkuu wa Chad N’Djamena kwa kuhudhuriwa na viongozi wa Ufaransa na wa mataifa ya magharibi wa Afrika.

Kikao hicho kimeanza katika hali ambayo, harakati za makundi ya kigaidi katika Ukanda wa Afrika Magharibi zimeshika kasi na kupanuka.

Katika miaka ya hivi karibuni, makundi ya kigaidi yamepanua uwepo wao katika maeneo mbalimbali ya magharibi mwa Afrika. Ukosefu wa uthabiti wa kisiasa wa nchi za kaskazini mwa Afrika hususan mazingira inayokabiliwa nayo Libya na kutokuweko serikali kuu katika nchi hiyo kwa ajili ya kuwa na usimamizi na udhibiti wa maeneo ya mipakani, kushindwa magaidi wa Daesh katika eneo la Asia Magharibi  na kukimbilia kwa wingi katika nchi mbalimbali za Kiafrika hususan za eneo la Sahel na Magharibi, hali mbaya ya kiuchumi ya nchi za Kiafrika, kuongezeka umasikini, ughali wa maisha,  kuweko nguvukazi ya vijana na kuweko mifumo wa kisiasa inayotetereka katika akthari ya nchi hizo ni mambo ambayo kivitendo yamezibadilisha nchi za bara hilo kuwa mahala pa harakati na usajili wa wanachama kunakofanywa na makundi ya kigaidi.

 

Hali hiyo katika nchi za Sahel Afrika hususan Mali na Nigeria imepelekea katika miaka ya hivi karibuni kushuhudiwe ongezeko la harakati za makundi ya kigaidi ndani ya nchi hizo na hata katika nchi za jirani. Kuongezeka ukosefu wa usalama na uthabiti wa kisiasa katika eneo hilo la Afrika, kumekuwa sababu ya kushadidi  uingiliaji wa madola ya kigeni hasa Ufaransa ambayo daima imekuwa na uwepo wa kikoloni katika akthari ya nchi za bara hilo.

Ufaransa mara hii imetuma wanajeshi wake huko Mali kwa kisingizio cha kusaidia juhudi za kulinda amani na baada ya miaka kadhaa mnamo mwaka 2014 kukaundwa kundi la nchi tano likibeba nara ya vita dhidi ya ugaidi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni kuwa, hadi kufikia sasa Ufaransa ina askari takribani 5,000 huko barani Afrika. Hata hivyo, licha ya madai ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo, wanajeshi hao hawajawa na mafanikio yoyote katika vita dhidi ya ugaidi katika eneo hilo na hata kuna kesi nyingi zinazoonyesha kuwa, askari hao wakati mwingine wamekuwa wakifanya mauaji dhidi ya raia hususan nchini Mali.

Uaransa ina askari wengi katika nchi ya Mali

 

Ushuhuda wa hilo ni shambulio la anga la hivi karibuni lililonasibishwa na Ufaransa dhidi ya sherehe ya harusi ambapo zaidi ya watu 100 waliuawa. Katika upande mwingine, makundi ya wanamgambo yangali yanadhibiti sehemu kubwa ya eneo la Sahel Afrika na yamekuwa yakifanya hujuma na mashambulio mtawalia dhidi ya vikosi vya serikali. Askari 6 walinda amani wameuawa nchini Mali tangu ulipoanza mwaka huu (2021) huku Ufaransa ikipoteza wanajeshi wake watano waliouawa mwezi Disemba mwaka jana.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, katika mapigano ya miezi ya hivi karibuni makumi ya wanajeshi na raia wa kawaida wameuawa huku zaidi ya raia milioni mbili wakilazimika kuwa wakimbizi. Jean-Herve Jezeque, Mkurugezi wa Kituo cha Kimataifa cha Migogoro wa Kimataifa anasema kuhusiana na hilo kwamba: Uingiliaji wa kijeshi haujaweza kutoa pigo kwa makundi ya kigaidi na wanamgambo. Hii ni kutokana na kuwa, wanamgambo hawa wana uwezo wa kurejea nyuma na kuvikwepa vikosi hivyo na kuendelea na hujuma na mashambulio yao.

Makundi ya wabeba silaha yamehatarisha usalama nchini Mali

 

Kikao hiki kinafanyika katika hali ambayo, bara la Afrika linakabiliwa na matatizo kama kushadidi opereseni za kigaidi zinazofanywa na makundi ya kufurutu ada, kusambaa virusi vya Corona, kushtadi umasikini, uhaba wa suhula za tiba na dawa, ukosefu wa uthabiti wa kisiasa na ufisadi unaoongezeka. Hii ni katika hali ambayo, utendaji wa vikosi vya Ufaransa pamoja na bajeti yao kubwa ambapo uwepo wa wanajeshi hao barani Afrika unasemekana kuwa unaigharimu Ufaransa takribani euro bilioni moja, suala ambalo hivi sasa limeibua malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali ya Macron.

Katika mazingira kama haya, kikao cha sasa cha kundi la nchi 5 kina umuhimu maalumu kama ambavyo Rais Emmanuel Macron amesafiri na kuelekea Chad kwa ajili ya kushiriki katika kikao hicho. Inaonekana kuwa, kikao cha kundi la nchi tano nchini Chad ni fursa kwa ajili ya kutathmini operesheni za kijeshi na kisiasa za nchi za kundi hilo katika kukabiliana na magaidi barani Afrika na kuchukua maamuzi kwa ajili ya mustakabali.  

Tags