Feb 23, 2021 14:06 UTC
  • Corona: Wasafiri kutoka Tanzania wapigwa marufuku kuingia nchini Oman

Wasafiri wanaoingia Oman kutoka nchi 10 wamepigwa marufuku ya kuingia katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Nchi zilizopigwa marufuku ni Tanzania Afrika Kusini, Lebanon, Sudan, Brazil, Nigeria, Guinea, Ghana, Sierra Leone, na Ethiopia.

Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa usiku wa Alkhamisi wiki hii na itadumu kwa muda wa siku 15.

Habari kutoka nchini Oman zinasema kuwa, hatua hiyo imetokana na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya udhitibi wa Corona nchini humo.

Kamati hiyo imesema kuwa, uamuzi huo ni wa kupambana na maambukizi ya Corona.

Marufuku hiyo pia inawahusisha watu watakaopita katika nchi hizo ndani ya siku 14 kabla ya kuingia Oman.

 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Oman, mkutano wa kamati hiyo uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Oman Hammoud bin Faisal Al Busaid.

Kamati hiyo imewataka wananchi wa Oman kutosafiri nje ya nchi ili kuzuia maambukizi na ikibidi kusafiri basi kuwe na sababu maalum. Marufuku hiyo inatatajiwa kuathiri pakubwa wasafiri kutoka Tanzania hasa kwa kutilia maanani kwamba, kuna watu wengi wanaosafiri kila siku kuelekea Oman wakitokea katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Tanzania iliacha kutangaza takwimu za maambukizi au vifo vya virusi hivyo mwezi Aprili mwaka jana baada ya maafisa wa maabara ya taifa kutuhumiwa kutoa matokeo yasiyo sahihi. Aidha Rais John Pombe Magufuli alitangaza Julai mwaka jana kwamba, Tanzania haina tena virusi vya Corona baada ya siku tatu za maombi ya kitaifa.