Feb 24, 2021 02:42 UTC
  • Sudan yataka upatanishi wa kimataifa kuhusu mgogogoro wa Bwawa la al-Nahdha

Waziri wa Umwagiliaji na Vyanzo vya Maji wa Sudan amesema kuwa, nchi yake inakusudia kuandaa uungaji mkono na upatanishi wa pande nne kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi mzozo wa Bwawa la al-Nahdha.

Yasir Abbas amesema kuwa, nchi yake imo mbioni kuimarisha upatanishi wa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Marekani ili pande hizo ziwe wapatanishi wa mgogoro unaoendelea kuhusiana na ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha katika Mto Nile.

Msimamo huo unatangazwa siku chache tu baada ya Abdalla Hamdok Waziri Mkuu wa Sudan kuashiria jinsi kadhia ya Bwawa la al-Nahdha ilivyogeuka na kuwa tishio kwa Wasudan milioni 20 na kusema kuwa, mgogoro wa ujenzi wa bwawa hilo unapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha

 

Kwa upande wake Ethiopia imeendelea kuzituhumu Sudan na Misri kwamba, ndizo zinazokwamisha mazungumzo ya kutatua hitilafu zilizopo baina ya nchi hizo tatu kuhusiana na Bwawa la al-Nahdha.

Bwawa la al-Nahdha limejengwa katika umbali wa kilomita 15 kutoka kwenye mpaka wa Ethiopia na Sudan. serikali ya Ethiopia inasema kuwa, karibu asilimia 80 ya ujenzi wa bwawa hilo umekamilika. Litakapoanza kufanya kazi bwawa hilo, litakuwa kituo kikuu zaidi cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji, duniani.

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini hayajakuwa na matokeo mazuri ya kuridhisha.

Tags