Feb 24, 2021 02:45 UTC
  • Waasi wa FDLR wa Rwanda wakana kuhusika na mauaji ya balozi wa Italia

Kundi la waasi wa Rwanda wa (FDLR), limekanusha kuhusika na mauaji ya balozi wa Italia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaliyotokea juzi Jumatatu.

Kanusho hilo la waasi linakuja masaa machache tu baada ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwatuhumu waasi wa FDLR wenye asili ya Rwanda, kwamba, walimshambulia na kumuua balozi wa Italia nchini humo Luca Attanasio hapo juzi karibu na mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, kundi la FDLR limekanusha kuhusika na shambulizi hilo, na kusema kuwa, vikosi vyake viko mbali na eneo la shambulizi hilo.

Bi Marie Ntumba Nzeza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametangaza kuwa, serikali ya Kinshasa tayari imeanzisha uchunguzi kubaini wahusika wa mauaji hayo na kwamba mpaka sasa hawajakamatwa.

Marie Ntumba Nzeza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Siku ya Jumatatu Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Italia ilithibitisha kuwa, balozi wa nchi hiyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameuawa katika shambulizi la makundi ya waasi mashariki mwa Congo.

Baada ya kupigwa risasi, balozi huyo wa Italia alikimbizwa hospitali na aliaga dunia kutokana na majeraha hayo.

Ripoti mbalimbali zinasema kuwa, eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja, na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.