Feb 24, 2021 11:59 UTC
  • Makumi ya wapiganaji wa Boko Haram wauawa nchini Nigeria

Kwa akali wapiganaji 81 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameuawa katika msito wa Sambisa nchini Nigeria kufuatia operesheni ya kijeshi ya vikosi vya mataifa kadhaa dhidi ya wanamgambo hao.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vimetangaza kuwa, mwanajeshi mmoja pia ameuawa katika operesheni hiyo na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Kikosi hicho kimefanikiwa pia kuwafurusha wanachama wengi katika eneo hilo la msitu wa Sambisa, ingawa waliondoka wakiwa wametega mabomu ya ardhi.

 Ripoti zaidi zinasema kuwa, hiyo ni moja ya operesheni kubwa iliyofanywa na kikosi cha mataifa kadhaa kinachopambana na wanamgambo hao wa Boko Haram ambao wamehatarisha maisha na usalama wa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria pamoja na maeneo ya nchi jirani.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria

 

Mwanzoni mwa mwezi huu Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alitangaza kuwa, mwaka huu wa 2021 ni mwaka wa mwisho wa uhai wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Rais Buhari ambaye amekuwa akikosolewa na duru za ndani na za nje kwa kushindwa kukabiliana na magaidi hao wa Boko Haram alisisitiza  hivi karibuni kuwa, kuliangamiza kundi hilo la kigaidi ni jukumu lake.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. 

Tangu wakati huo hadi sasa kundi hilo limeua watu wapatao 36 elfu na kusababisha raia wengine zaidi ya milioni mbili pia kuwa wakimbizi katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.