Feb 24, 2021 12:01 UTC
  • Rais Kagame: Kuna  undumakuwili katika usambazaji wa chanjo ya corona duniani

Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema kuwa, kuna undumakuwili na unafiki katika usambazaji wa chanjo ya Covid-19 duniani.

Rais Kagame amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus kusema kwamba, mkataba ulioafikiwa kati ya mataifa tajiri na watengenezaji wa chanjo umefanya kuwa vigumu kwa shirika hilo kupata chanjo kwa ajili ya mpango wake wa COVAX.

Rais Paul Kagame amesema kuwa, huu ni unafiki na undumakuwili ambao siku zote tumekuwa tukiuzungumzia. Kadhalika Rais huyo wa Rwanda amesisitiza kuwa, huu ni mfano mmoja tu kati ya mifano mingi iliyopo kuhusiana na undumakuwili huu.

Chanjo ya Corona

 

Mpango wa COVAX umeanzishwa ili kuhakikisha nchi tajiri duniani hazihodhi dozi zote za chanjo ya corona ambazo kwa sasa zinapatikana kwa kiwango maalum na kutoweza kukidhi mahitaji ya ulimwengu mzima.

Mpango huo unasimamia pia utaratibu wa kupatia fedha na kuandaa mazingira kwa nchi 92 zenye kipato cha chini na cha kati duniani ya kuweza kupata chanjo hiyo ya kujikinga na maradhi ya Covid-19.

Mataifa tajiri yameendelea kosolewa katika pembe mbalimbali za dunia kutokana na hatua yao ya kuhodhi chanjo na kufanya kuwa vigumu kwa nchi masikini kupata chanjo yoyote.