Feb 25, 2021 07:27 UTC
  • Watu 10 wauawa katika shambulio la Boko Haram Maiduguri, Nigeria

Watu wasiopungua 10 wanaripotiwa kuuawa katika mji wa Maiduguri uliopo katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vimethibitisha kutokea shambulio hilo na kusema kuwa, watu wengie 60 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi la wanamgambo hao wa Boko Haram ambalo lilitekelezwa kupitia milipuko kadhaa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, jana vyombo vya usalama vya Nigeria viliripoti kuwa, kwa akali wapiganaji 81 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameuawa katika msitu wa Sambisa nchini Nigeria kufuatia operesheni ya kijeshi ya vikosi vya mataifa kadhaa dhidi ya wanamgambo hao.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram

 

Ripoti zaidi zinasema kuwa, hiyo ni moja ya operesheni kubwa iliyofanywa na kikosi cha mataifa kadhaa kinachopambana na wanamgambo hao wa Boko Haram ambao wamehatarisha maisha na usalama wa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria pamoja na maeneo ya nchi jirani.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. 

Tangu wakati huo hadi sasa kundi hilo limeua watu wapatao 36 elfu na kusababisha raia wengine zaidi ya milioni mbili pia kuwa wakimbizi katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.