Feb 25, 2021 07:28 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Hali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati bado ni ya hatari

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, hali ya amani na utulivu haijarejea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kwamba, kungali kunashuhudiwa machafuko katika nchi hiyo.

Hayo yameelezwa na Jean-Pierre Lacroix Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ulinzi wa amani alipokuwa akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kubainisha kwamba, licha ya uchaguzi wa rais nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kufanyika kwa mafanikio na kuwepo kwa maendeleo mengine ya maana, lakini hali ya nchi hiyo bado inaendelea kutawaliwa na vurugu na hatari.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, kukosekana kwa usalama kumezuia kupitishwa kwa malori zaidi ya 1,000 yaliyobeba msaada wa kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na chakula na dawa, na vifaa vya kupambana na janga la COVID-19.

Waasi wa Kikristo wa Anti-Balaka

 

Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2016 hadi sasa Rais  Faustin-Archange Touadéra amekuwa akifanya jitihada kuhakikisha maeneo mengi makubwa ya nchi hiyo yanayoshikiliwa na makundi ya wanamgambo yanarejea kwenye udhibiti wa serikali.