Feb 25, 2021 07:36 UTC
  • Mchakato wa uteuzi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wazusha hitilafu

Mchakato wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa kujaza nafasi ya Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Liberat Mfumukeko anayemaliza muhula wake mwezi Aprili, unazidi kuibua hisia kali ambapo mataifa wanachama yanaendelea kuvutana kuelekea kukamilika mchakato huo.

Hali hii imejitokeza baada ya Kenya na Sudan Kusini, kutangaza azma ya kuteua mwaniaji kwenye nafasi hiyo ya juu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa kawaida nafasi hiyo huwa ni ya kupokezana kati ya mataifa wanachama na japokuwa mara hii ni zamu ya Kenya kujaza nafasi hiyo, lakini Sudan Kusini taifa la hivi majuzi kujiunga na jumuiya limetangaza lipo kwenye kinyanganyiro hicho.

Hatua hiyo ya Sudan Kusini imezusha maswali mengi na huenda ikaibua mgogoro katika jumuiya hiyo muhimu ya kieneo.

Liberat Mfumukeko, raia wa Burundi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayemaliza muda wake

 

Hii ni licha ya  Sudan Kusini kutuhumiwa kuwa na deni kubwa la  ada ya uanachama na  bado haijapitisha sheria  hitajika za kuwezesha biashara huru na umoja wa forodha.

Wanaotazamiwa kuwania kiti hicho kutoka Kenya ni katibu mtendaji katika wizara ya mambo ya nje Ababu Namwamba, Waziri wa ustawi wa jumuiya ya Afrika Mashariki Aden Mohammed  na Waziri wa Michezo Amina Mohammed.

Sudan Kusini kwa upande wake ,imempendekeza aliyekuwa waziri wa fedha Aggrey Tisa Sabuni kkwa ajili ya kuwania kumrithi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayemaliza muda wake mwezi Aprili.