Feb 27, 2021 07:02 UTC
  • Majina ya mawaziri wa serikali ya mpito ya Libya yawasilishwa bungeni kupigiwa kura ya imani

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Libya amewasilisha bungeni majina ya mawaziri aliowapendekeza kwa ajili ya kuunda serikali kwa madhumuni ya kuhitimisha hali ya mchafukoge nchini humo.

Abdulhamid al Dadaiba amependekeza kwa bunge kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kulingana na mchakato wa amani wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, ofisi ya waziri mkuu huyo wa mpito wa Libya imesema, kabla ya majina ya waliopendekezwa kuunda baraza la mawaziri kuwasilishwa bungeni, yalitazamiwa kufikishwa kwanza kwa Baraza la Urais la nchi hiyo.

Tangazo lililotolewa na ofisi hiyo limeeleza kuwa, bunge litakuwa na fursa hadi tarehe 19 ya mwezi ujao wa Machi ya kuwapigia kura ya kuwa na imani nao mawaziri wateule wa serikali ya mpito; na baada ya hapo serikali ya muda ya waziri mkuu Abdulhamid al Dadaiba itapaswa ianze kuyashughulikia matarajio ya wananchi wa Libya wanaokabuliwa na uhaba wa mzunguko wa fedha, fueli, tatizo la kukatwa umeme na ughali wa bidhaa.

Abdulhamid al Dadaiba

Itakumbukwa kuwa baada ya kupigwa kura katika kikao cha baraza la mazungumzo ya Libya kilichofanyika mjini Geneva chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, Abdulhamid al-Dabaiba alichaguliwa waziri mkuu, Mohamed Yunus al-Menfi alichaguliwa mkuu wa baraza la urais na Musa Al Koni  na Abdullah Hussein Al Lafi walichaguliwa kuwa wajumbe wawili wa baraza hilo.

Shakhsia hao walioshinda katika zoezi hilo la upigaji kura lililofanyika katika mazungumzo ya Geneva, watabeba jukumu la kuiongoza Libya kwa muda, hadi uchaguzi wa rais na bunge ambao umepangwa kufanyika Septemba 24 mwaka huu.../

Tags