Mar 02, 2021 10:50 UTC
  • Wafanyakazi wanne wa sekta ya habari watiwa mbaroni katika eneo  la Tigray, Ethiopia

Wafanyakazi wanne wa sekta ya habari katika eneo lililoathiriwa na machafuko la Tigray nchini Ethiopia wametiwa mbaroni na kushikiliwa korokoroni. Hayo yameelezwa na familia na wafanyakazi wenzao.

Eneo la Tigray limekuwa kitovu cha mapigano tangu mwezi Novemba mwaka jana pale Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, alipotangaza oparesheni za jeshi dhidi ya Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) baada ya kuwatuhumu wapiganaji wa harakati hiyo kuwa wameshambulia kambi za jeshi la Ethiopia.

Wanahabari wamekuwa wakikabiliana na vizuizi na hali ngumu wakati wa kuripot matukio ya eneo la Tigray, huku huduma za intaneti zikikatwa mara kwa mara katika eneo hilo.

Serikali ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ilitangaza ushindi dhidi ya harakati ya TPLF baada ya wapiganaji wa kundi hilo kuondoka katika miji mikubwa mwishoni mwa mwezi Novemba. Hata hivyo mapigano ya hapa na pale yamekuwa yakiendelea katika baadhi ya sehemu za Tigray.  

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia  

Taasisi saba za kimataifa za habari ikiwemo televisheni ya al Jazeera ya Qatar tayari zimepatiwa kibali cha kuripoti matukio ya Tigray, lakini waandishi habari kiujumla wametahadharishwa na maafisa wa serikali kwamba watakabiliwa na hatua mbalimbali  iwapo hawatakidhi vigezo vilivyoainishwa. 

Fitsum Berhane na Alula Akalu ambao walikuwa wakifanya kazi kama wakalimani wa shirika la habari la AFP na gazeti la Financial Times walikamatwa Jumamosi iliyopita huku mwandishi habari wa tatu, Temrat Yemane, akitiwa mbaroni huko Mekelle makao makuu ya eneo la Tigray. Jana Jumatatu shirika la habari la BBC liliripoti kuwa, ripota wake, Girmay Gebru ametiwa nguvuni na jeshi huko Mekelle. 

Fitsum na Alula wanashikiliwa katika chuo cha kijeshi karibu na Chuo Kikuu cha Mekelle. Hayo yameelezwa na familia za wanahabari hao kwa shirika la habari la AFP. Wamesema waandishi habari hao wako chini ya uchunguzi na hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa hadi sasa kuhusu sababu za kutiwa kwao mbaroni. 

Tags