Mar 05, 2021 02:32 UTC
  • UN: Majeshi ya Eritrea, Ethiopia yumkini yamefanya jinai za kivita Tigray

Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema ofisi yake ina ithibati ya kufanyika jinai za kutisha ambazo zinaweza kuwa jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea katika eneo la Tigray.

Michelle Bachelet alisema hayo jana Alkhamisi katika taarifa ambapo ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi huru wa hali ya eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia, ambalo limeshuhudia mapigano kwa miezi kadhaa.

Amesema pande kadhaa za mapigano hayo zimeshatambuliwa wakiwemo askari wa Jeshi la Ulinzi la Ethiopia, Jeshi la Taifa la Eritrea, Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray (TPLF), vikosi vya eneo la Amhara na waitifaki wao.

Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema ofisi yake imethibitisha pia ripoti za mauaji ya halaiki katika miji ya Axum, na Dengelat ya katikati mwa Tigray, yaliyofanywa na wanajeshi wa Eritrea mwishoni mwa mwaka jana.

Taarifa ya taasisi hiyo ya UN imekuja siku chache baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amesty International kusema mauaji ya kiholela ya mamia ya raia yaliyofanywa na jeshi la Eritrea katika mji wa kale wa Ethiopia wa Axum Novemba mwaka jana ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na ukanyagaji wa sheria za kimataifa za kumlinda mwanadamu.

Michelle Bachelet

Ripoti ya Amnesty International imesema kuwa, mnamo Novemba 28 na 29 mwaka uliopita 2020, wanajeshi wa Eritrea kwa makusudi na mpangilio maalumu waliwaua mamia ya raia katika mji huo wa Axum, yapata kilomita 187 kaskazini mwa Makelle, makao makuu ya eneo la Tigray.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wameuawa na wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo ya eneo la Tigray. 

Tags