Mar 05, 2021 02:38 UTC
  • Wahajiri 20 waaga dunia baada ya kugharikishwa baharini Djibouti

Makumi ya wakimbizi na wahajiri wamekufa maji baada ya wafanya magendo ya binadamu kuwarusha baharini nchini Djibouti.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM), wahajiri zaidi ya 20 wamepoteza maisha baada ya kugharikishwa majini na wafanya magendo, wakiwa katika boti iliyokuwa imejaa kupindukia ikilekea nchini Yemen kutoka Djibouti, mashariki mwa Afrika.

Taarifa ya IOM imesema kuwa, wafanya magendo hao waliwarusha baharini wakimbizi na wahajiri haramu zaidi ya 80, baada ya kuhisi kuwa safari hiyo ingelishindikana kwa kuwa boti waliyokuwa wakisafiria ilikuwa imebeba watu zaidi ya 200.

Wahamiaji haramu raia wa Somalia na Ethiopia wamekuwa wakiaga dunia katika ajali hatarishi za namna hii za kujaribu kwenda Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, wakikimbia makali ya njaa, umaskini na vita katika nchi zao.

Wahajiri katika safari hatarishi ya baharini

Oktoba mwaka jana 2020, wahajiri wanane wa Kiafrika waliaga dunia baada ya wafanya magendo kuwalazimisha kuondoka kwenye boti na kuruka majini karibu na Djibouti.

Mwaka 2017, wahamiaji haramu zaidi ya 50 raia wa Ethiopia na Somalia waliaga dunia baada ya 'kugharikishwa kwa makusudi' na wafanya magendo katika Pwani ya Yemen.

Tags