Mar 05, 2021 12:24 UTC
  • Kenya yazindua kampeni ya kitaifa ya chanjo ya kupambana na corona

Kenya hii leo imezindua kampeni ya kitaifa ya chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, huku Patrick Amoth, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya akiwa Mkenya wa kwanza kuchanjwa katika ardhi ya nchi hiyo.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi, ambapo wahudumu wengine watatu wa afya wa hospitali hiyo wamepigwa chanjo hiyo.

Dakta Amoth amesema Kenya inapania kuwachanja watu milioni 1.25 kufikia Juni 30 mwaka huu katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo iliyozinduliwa leo. Ameongeza kuwa, katika awamu ya pili inayotazamiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu, serikali ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki inalenga kuwachanja Wakenya milioni 9.6.

Usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii, shehena ya dozi milioni 1.02 za chanjo ya AstraZeneca kutoka Taasisi ya Serum India iliwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi.

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe amesema Kenya haijashinda vita dhidi ya janga la Covid-19 licha ya chanjo ya kukabiliana na corona kuwasili nchini humo. Shehena nyingine ya chanjo ya corona inatazamiwa kuwasili nchini humo kufikia mwishoni mwa mwezi huu au mapema Aprili.

Hapo jana pia, Rais Uhuru Kenyatta aliwahimiza wananchi wa Kenya kutilia mkazo sheria na mikakati iliyowekwa ili kusaidia kudhibiti msambao wa maradhi hayo hatarishi ambayo yameua watu karibu elfu mbili kufikia sasa nchini humo.

Tags