Mar 05, 2021 12:29 UTC
  • Magaidi 52 wa al-Shabaab wauawa katika shambulio dhidi ya jela nchini Somalia

Wanamgambo wasiopungua 52 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa katika shambulio la wapiganaji hao dhidi ya jela moja iliyoko katika jimbo la Puntland,kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo magaidi hao wamefanikiwa kuwatorosha jela wenzao zaidi ya 400 waliokuwa wakikabiliwa na mashitaka na vifungo mbalimbali katika jela kuu ya mji wa Bosaso jimboni hapo.

Hussein Ali Muhamud, Kamanda wa Polisi katika eneo la Bari amethibitisha habari ya kutokea hujuma hiyo na kubainisha kuwa, maafisa usalama wanane wameuawa katika tukio hilo la usiku wa kuamkia leo.

Kundi la al-Shabaab kupitia radio yake ya kipropaganda ya Andalusia limedai kuwa limepata ushindi mkubwa katika shambulio hilo, na eti limewatorosha jela mamia ya wafuasi wake wakiwemo makamanda wa ngazi za juu wa genge hilo.

Hata hivyo vyombo vya usalama katika eneo hilo vinasema aghalabu ya wafungwa waliotoroshwa jela na al-Shabaab wamekamatwa tena na wako kizuizini.

Baadhi ya wananchama wa al-Shabaab ya Somalia

Genge hilo la ukufurishaji lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limedai kuwa baadhi ya wafungwa liliowatorosha jela ni wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab limekuwa likiendesha kampeni ya mtutu wa bunduki kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia.

 

Tags