Mar 06, 2021 08:14 UTC
  • 4 wauawa katika maandamano ya kupinga kukamatwa kinara wa upinzani Senegal

Kwa akali watu wanne wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya ghasia ya kulalamikia kitendo cha maafisa usalama kumtia mbaroni kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Senegal.

Maandamano hayo yalishtadi jana Ijumaa, baada ya kinara wa upinzani Ousmane Sonko kufikishwa mahakamani akiandamwa na tuhuma za ubakaji na kutoa vitisho. Mawakili na wafuasi wa mwanasiasa huyo wa upinzani wamepinga vikali madai hayo, wakisisitiza kuwa kiongozi huyo amebabambikiwa kesi hizo.

Maandamano hayo ya ghasia yaliyoanza tokea Jumatano katika mji mkuu Dakar na kusambaa katika miji mingine ya nchi hiyo, yanahesabiwa kuwa mabaya zaidi nchini humo katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita.

Hapo jana vyombo vya dola vilizima huduma za mitandao ya kijamii kama Facebook. Akthari ya wafuasi wa mwanasiasa huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 46 ni vijana.

Rais wa Senegal

Serikali ya Rais Macky Sall wa Senegal imekuwa ikikosolewa kwa kuwabinya na kuwafumba midomo wapinzani nchini humo. Viongozi wengine wa upinzani ambao wamekuwa wakilengwa kwa tuhuma za kutenda jinai ni Meya wa zamani wa mji mkuu, Dakar, Khalifa Sall na Karim Wade, mtoto wa kiume wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdoulaye Wade; wanasiasa ambao walizuiwa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2019.

Septemba mwaka jana, Rais Macky Sall alitangaza msahama kwa kiongozi wa upinzani nchini humo, Khalifa Sall ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano jela tokea mwaka 2018 baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya ufisadi iliyokuwa ikimkabili.

 

 

 

Tags