Mar 06, 2021 08:15 UTC
  • Baraza la Usalama laendelea kufumbia macho mapigano Tigray, Ethiopia

Jitihada za kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litoe taarifa ya kutaka kusitishwa machafuko na mauaji yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia zimegonga mwamba.

Hii ni baada ya rasimu ya taarifa hiyo iliyoandaliwa na Ireland kupingwa na nchi kadhaa wanachama wa Baraza la Usalama la UN zikiwemo India, China na Russia.

Wanadiplomasia watatu katika chombo hicho cha UN wamenukuliwa na shirika la habari la AP wakisema kuwa, Ireland hapo jana iliamua kutoshinikiza kutolewa taarifa hiyo ya kulaani jinai za Tigray, baada ya nchi kadhaa wanachama wa Baraza la Usalama kupuuzilia mbali wazo hilo.

Hiyo ndiyo ingelikuwa taarifa ya kwanza kutolewa na taasisi hiyo ya juu kabisa ya Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Tigray, tokea uanze miezi minne iliyopita.

Malaki wawa wakimbizi kutokana na mapigano eneo la Tigray

Hii ni katika hali ambayo, Alkhamisi iliyopita, Michelle Bachelet, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema ofisi yake ina ithibati ya kufanyika jinai za kutisha ambazo zinaweza kuwa jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea katika eneo la Tigray.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wameuawa na wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo ya eneo la Tigray. 

Tags