Mar 08, 2021 07:42 UTC
  • Skuli zafungwa kwa muda wa juma zima Senegal kufuatia mapigano na machafuko

Skuli zimefungwa kwa muda wa juma zima nchini Senegal kutokana na mapigano na machafuko yaliyozuka hivi karibuni nchini humo.

Maafisa wa serikali walitangaza jana kuwa, skuli nchini humo zitafungwa kwa muda wa wiki moja kuanzia leo kufuatia mapigano na machafuko yaliyoanza wiki iliyopita katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo na kuvuruga shughuli za masomo.

Uamuzi huo umechukuliwa huku harakati ya upinzani ya kutetea demokrasia inayojumuisha chama kikuu cha upinzani cha Pastef ikiwa imetoa mwito kwa wananchi kuandamana kwa muda wa siku tatu mtawalia kuanzia leo.

Mwito huo umetolewa baada ya siku kadhaa za mapambano baina ya wafuasi wa upinzani na askari polisi yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua watano hadi sasa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Ousmane Sonko

Machafuko nchini Senegal yalianza siku ya Jumatano iliyopita baada ya polisi kumtia nguvuni Ousmane Sonko alipokuwa anaelekea mahakamani kujibu shtaka la ubakaji, ambalo mwenyewe anasema limetokana na sababu za kisiasa.

Sonko mwenye umri wa miaka 46, ni mwanasiasa mwenye umaarufu mkubwa kwa tabaka la vijana nchini Senegal, anayeonekana kutoa upinzani mkubwa kwa rais wa nchi hiyo Macky Sall licha ya kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2019. Kiongozi huyo wa upinzani anatazamiwa kufika mahakamani leo kujibu shtaka hilo la ubakaji linalomkabili.../

Tags