Mar 11, 2021 07:18 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ivory Coast Hamed Bakayoko afariki kwa saratini akiwa na umri wa miaka 56

Waziri Mkuu wa Ivory Coast Hamed Bakayoko amefariki dunia kwa maradhi ya saratani katika hospitali moja mjini Freiburg nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Ivory Coast imeeleza kuwa, Bakayoko aliaga dunia jana, siku mbili baada ya kutimiza umri wa miaka 56 na takriban miezi minane tangu kilipotokea kifo cha mtangulizi wake.

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast ametuma ujumbe kwenye ukurasa wa twitter usemao: "Nchi yetu iko kwenye maombolezo."

"Kwa majonzi makubwa ninatangaza kifo cha Waziri Mkuu Hamed Bakayoko, kiongozi wa nchi, waziri wa ulinzi... kilichotokea Ujerumani kutokana na saratani", imeeleza sehemu ya ujumbe wa Ouattara akimuelezea Bakayoko kuwa ni kiongozi mkubwa wa nchi, mfano wa kuigwa na vijana na shakhsia mwenye ukarimu mkubwa na uaminifu wa kupigiwa mfano.

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast

Msemaji wa chama cha upinzani cha Harakati ya Wananchi ya Ivory Coast Issiaka Sangare amemtaja hayati Hamed Bakayoko kuwa ni kiungo kikuu katika ulingo wa siasa na mdau mkubwa katika maridhiano.

Bakayoko, ambaye ni mtu wa karibu wa Rais Alassane Ouattara aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Ivory Coast Julai 2020 kufuatia kifo cha ghafla cha mtangulizi wake Amadou Gon Coulibaly.

Alisafirishwa kupelekwa Ufaransa Februari 18 kufanyiwa uchunguzi wa kitiba na baadaye akahamishiwa katika hospitali ya Freiburg, mji ulioko kusini magharibi mwa Ujerumani.

Ijumaa iliyopita, serikali ya Ivory Coast ilieleza katika taarifa kwamba Rais Ouattara alikutana na Bakayoko wakati wa ziara yake nchini Ufaransa na kutokana na hali yake ya kiafya ikashauriwa muda wake kuwepo hospitalini waziri mkuu huyo urefushwe.

Siku ya Jumatatu, Rais wa Ivory Coast alimteua mwandani wake na mkuu wa Ikulu Patrick Achi kuwa waziri mkuu wa muda kukaimu nafasi ya Bakayoko.../

Tags