Mar 14, 2021 02:39 UTC
  • UN yatilia mkazo umuhimu wa kufanyika uchaguzi  kama ilivyopangwa nchini Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kuitaka serikali ya Somalia kuitisha uchaguzi mkuu kama ilivyopangwa na bila ya kuuchelewesha.

Katika azimio hilo, Baraza la Usalama limeelezea hofu yake kutokana na kuakhirisha uchaguzi mkuu Somalia na limeitaka serikali ya shirikisho ya nchi hiyo pamoja na serikali za majimbo, kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki unafanyika nchini humo kama ilivyokubaliwa katika makubaliano ya tarehe 17 Septemba 2020.

Baraza hilo limepongeza mafanikio yaliyiopatikana huko Somalia na kukumbusha kuwa, vitisho vya kiusalama kutoka kwa genge la kigaidi la al Shabab na magenge mengine yenye misimamo mikali bado vipo nchini Somalia.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Hatua hiyo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imekuja ikiwa ni sehemu ya mashinikizo kwa Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia baada ya kushindwa kuitisha uchaguzi wa rais tarehe 8 mwezi uliopita wa Februari. Uchaguzi huo haukufanyika baada ya kukosekana mwafaka wa namna ya kuuendesha. Majimbo mawili ya Somalia yalisema hayawezi kushiriki kwenye uchaguzi huo bila ya kufikiwa kwanza makubaliano maalumu.

Wakosoaji wanamtupia lawama Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wakidai kuwa ndiye anayekwamisha kufanyika uchaguzi nchini humo. Wanamshutumu kuwa anafanya njama za kurefusha kipindi chake cha kubakia madarakani. Hata hivyo rais huyo wa Somalia anakanusha shutuma hizo akilaumu madola ya kigeni yanayoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kuwa ndiyo yanayokwamisha uchaguzi Somalia.

Tags