Mar 17, 2021 04:33 UTC
  • Save the Children: Magaidi wanaua watoto kwa kuwachinja Msumbiji

Shirika la misaada ya kibinadamu la Save the Children limesema wanachama wa magenge ya kigaidi katika mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji wanaua watoto wadogo kikatili kwa kuwakata vichwa.

Katika ripoti yake, Save the Children imesema imezihoji familia za wakimbizi wa ndani katika mkoa huo, ambazo zimesema magaidi hawawasazi hata watoto wadogo na wanaua hata wenye miaka 11 kwa kuwachinja.

Chance Briggs, Mkurugenzi wa Shirika la misaada ya kibinadamu la Save the Children amesema ripoti za kushambuliwa watoto wadogo na kuuawa kikatili zinakirihisha na kuhuzunisha sana.

Mwanamke mmoja ameliambia shirika hilo kuwa, alilazimika kutazama mwanawe wa kiume wa miaka 12 akiuawa kikatili na magaidi hao.

Magaidi wa Msumbiji waliotangaza utiifu wao kwa ISIS

Mwishoni mwa mwaka jana 2020, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilisema takribani watoto 250,000 wamekimbia makazi yao kutokana na hujuma za kigaidi zinazoendelea kwenye jimbo hilo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji. Eneo la Cabo Delgado lenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi limekuwa likilengwa na magaidi tangu mwaka 2017.

Watu zaidi ya 2,500 wameuliwa katika vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017, kutokana na mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.

Tags