Mar 18, 2021 07:14 UTC
  • Mtetemeko mkubwa wa ardhi waikumba Algeria mapema leo afajiri

Mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa daraja 6 kwa kipimo cha rishta umetokea katika eneo la kaskazini mashariki mwa mji wa Bejaia, katika umbali wa kilomita 10 chini ya ardhi huko Algeria.

Sehemu hasa ulipotokea mtetemeko huo ni eneo lililoko umbali wa kilomita 20 kaskazini mashariki mwa mji huo wa Bejaia wenye wakazi 164,000. Mtetemeko huo umehisika katika maeneo mengi, hadi katika mji mkuu Algiers. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa, baada ya mtetemeko huo, kumetokea mitetemeko mingine miwili mikubwa; mmoja wa daraja 5.2 na mwingine wa daraja 4.7 kwa kipimo cha rishta mbali na mitetemeko mingine kadhaa midogo midogo.

Habari kutoka katika mji wa Bejaia zinasema kuwa, watu wamechanganyikiwa, wametoka kwa pupa katika nyumba zao na kukimbilia kwenye maeneo ya wazi.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, kumetokea hasara na madhara mengi kama vile majengo kuporomoka na kuathiriwa vibaya. Hata hivyo ni mapema mno kuweza kujua hasara hasa zilizosababishwa na mitetemeko hiyo.

Picha zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii nazo zinaonesha baadhi ya madhara yaliyosababishwa na mitetemeko hiyo ingawa kunatarajiwa kutolewa taarifa zaidi kadiri muda unavyopita.

Tags