Mar 22, 2021 12:32 UTC
  • Viongozi wa Afrika wamlilia hayati Magufuli Dodoma; Kenyatta asimamisha hotuba kwa kusikia adhana

Viongozi na marais kutoka nchi 17 duniani hususan za Afrika wamehudhuria shughuli ya kitaifa ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli iliyofanyika leo Jumatatu katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi amesema hayati John Magufuli alikuwa mpiganaji na mzalendo, mtetezi mkuu wa uhuru wa utamaduni na kiuchumi barani Afrika. Tshisekedi ameyasema hayo leo Jumatatu katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma wakati wa kuuaga mwili wa hayati Magufuli.

Amesema kuondoka kwake kumetikisa Bara la Afrika kwa kuwa ni mwanasiasa mkongwe aliyeboresha maisha na kujali wananchi wake, kutetea na kuendeleza uchumi.

Rais Tshisekedi wa DRC

Huku hayo yakiarifiwa, Rais wa Kenya,  Uhuru Kenyatta amesimamisha hotuba yake kwa dakika moja kupisha wito wa Swala (adhana) ya adhuhuri wakati akitoa salamu za pole kwa Watanzania katika shughuli hiyo ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania.

Katika hotuba yake Kenyatta amemuomba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuendeleza falsafa ya 'Hapa Kazi Tu' aliyoiacha Magufuli kwa kuwa inawafanya Watanzania kuwa na moyo wa ushujaa na kusonga mbele. Amesema Dkt. Magufuli amelifunza bara la Afrika kuwa linaweza kustawi na kuimarika bila kutegemea misaada ya nchi ajinabi.

Kwa upande wake, Rais wa Zambia Edgar Lungu ameelezea kuumizwa na kifo cha rafiki yake hayati Magufuli huku akielezea namna mwendazake alivyolinyanyua taifa la Zambia kiuchumi kupitia reli ya  Tazara.

Rais Kenyatta alpokutana na hayati Magufuli huko nyuma

Naye Rais wa Botswana,  Mokgweetsi Masisi amesema John Magufuli ataendelea kukumbukwa kwa michango yake katika kuiunganisha  Afrika. 

Wakati huohuo, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ametaja mambo matatu akimshukuru aliyekuwa Rais wa Tanzania,  Hayati John Magufuli  ikiwemo kumweleza umuhimu wa lugha ya Kiswahili na kuanza kufundishwa nchini Afrika Kusini. Ameyataja mambo hayo kuwa ni kusimama maadili, rushwa na ubadhirifu na  kuitangaza lugha ya Kiswahili.

Magufuli alifariki dunia Machi 17 kutokana na maradhi ya moyo. Rais huyo wa awamu ya tano anatarajiwa kuzikwa Machi 26 nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Tags