Mar 23, 2021 14:40 UTC
  • Wazanzibar wajitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa hayati Magufuli katika Uwanja wa Amaan

Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi leo Jumanne ameongoza viongozi mbalimbali na Wazanzibari kwa ujumla katika shughuli ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Dkt John Pombe Magufuli, ambaye alifariki dunia Machi 17 jijini Dar es Salaam.

Viongozi wakuu wa serikali, mashirika ya kimataifa, mabalozi wadogo waliopo Zanzibar pamoja na viongozi wa taasisi binafsi wamejitokeza kwa wingi katika shughuli hiyo ya kuuaga mwili wa Dkt Magufuli.

Mapema leo, Dkt Mwinyi aliongoza viongozi mbalimbali kuupokea mwili wa Magufuli katika Uwanja wa Ndege wa Aman Abeid Karume visiwani Zanzibar, ukitokea Dodoma, ambako uliagwa jana na viongozi wa ndani na nje ya Tanzania.

Mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania hayati John Magufuli utalala Ikulu Zanzibar leo Jumanne na kesho asubuhi utapelekwa mkoani Mwanza. Hayo yameelezwa leo na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akizungumza kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar ilikofanyika shughuli ya kumuaga Dkt Magufuli.

Amesema, “Zanzibar mtapata fursa ya kila mmoja kupita kumuaga, hata kama tutamaliza saa sita usiku ili mradi mkate kiu ya kumuaga. Kesho asubuhi mwili utaondoka kwenda Mwanza na kesho utatembea kwa gari kupita daraja la Busisi na kisha kusimama kwa dakika 10 nyumbani kwa wazazi wa mke wa marehemu.” 

Wazanzibari walivyojitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa Dkt Magufuli

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amesema mapokezi ya leo Zanzibar yamedhihirisha umoja na mshikamano. Amefafanua kuwa,  “Ndugu zetu wa Zanzibar wameudhihirishia ulimwengu kuwa sisi ni ndugu wa damu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awabariki wananchi wa pande zote mbili za muungano ili tuzidi kushikamana.”

Wakati huohuo, Umoja wa mataifa (UN) umesema bendera ya umoja huo itapepea nusu mlingoti katika ofisi za makao makuu jijini New York Marekani siku ya Ijumaa Machi 26, kumuenzi Rais John Magufuli ambaye siku hiyo ndiyo atazikwa wilayani Chato Mkoa wa Geita.

Tags