Apr 05, 2021 12:54 UTC
  • Viongozi wa Somalia washindwa kukubaliana juu ya ajenda ya mkutano muhimu wa uchaguzi

Viongozi wa Somalia wameshindwa kufikia makubaliano juu ya ajenda kuu ya mkutano muhimu wa uchaguzi, suala ambalo limedhihirisha tena ufa uliopo kati ya makundi ya kisiasa ya Somalia.

Viongozi hao wameahidi kukutana tena Jumanne ya kesho kujadili suala hilo, kicha ya kwamba nchi hiyo inaendelea kuchelewa sana kuitisha uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa kufanyika Februari mwaka huu.

Mkutano huo ulijumuisha Rais Mohamed Farmaajo na viongozi wa majimbo makuu 5 (FMS) pamoja na Gavana wa jimbo la Benadir, linalojumuisha jiji kuu la Mogadishu.

Mazungumzo hayo yaliyofunguliwa na Rais Farmaajo wa Somalia Jumapili alasiri yalitarajiwa kuwa 'hatua ya mwanzo', kwani vyama vya siasa vya Somalia vinaendelea kutawaliwa na hali ya kutoaminiana. 

Rais Farmaajo wa Somalia

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza katika kipindi cha wiki tatu zilizopita baina ya wakuu wote wa serikali ya shirikisho, ingawa wote walifika Mogadishu wiki tatu kabla. 

Viongozi wa majimbo ya Puntland na Jubaland hapo awali walikuwa wamemshutumu Rais Farmaajo kwa kupotosha ajenda ya mazungumzo ya Wasomali kwa faida zake binafsi.

Washirika wa kimataifa wa Somalia wamekuwa wakiwashinikiza viongozi wa nchi hiyo kufikia makubaliano juu ya mtindo wa uchaguzi ulioainishwa tarehe 17 Septemba  2020, na hivyo kutayarisha njia ya kufanyika uchaguzi wa moja kwa moja nchini Somalia ili kuchagua wabunge na maseneta 53. 

Tags