Apr 07, 2021 02:34 UTC
  • Kuendelea mgogoro nchini Algeria; kususiwa uchaguzi wa Bunge na vyama vya siasa

Mgogoro wa kisiasa nchini Algeria ungali unaendelea kufukuta kwani licha ya juhudi za serikali za kutuliza hali ya mambo na kuitisha uchaguzi wa Bunge wa mapema, lakini vyama vinne vya siasa vya nchi hiyo vimetangaza kususia uchaguzi huo.

Vyama vya siasa vya Socialist Forces Front (FFS) na Rally for Culture and Democracy and Workers vimetoa taarifa kwa nyakati tofauti vikisisitiza kwamba, havitashiriki uchaguzi huo ujao wa Bunge.

Chama cha Socialist Forces Front (FFS) kimesema katika taarifa yake kwamba, masharti na vigezo vya kufanyika uchaguzi huo wa Bunge wa Juni 12 mwaka huu havijatimia na kwamba, kufanyika uchaguzi huo siyo tiba mujarabu ya kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo ambao una chimbuko na sababu mbalimbali.

Vyama vya upinzani nchini Algeria vinaitaka serikali iwaache wananchi wa nchi hiyo wajiainishie mustakabali wao, iruhusu kufanyika harakati za kisiasa na kijamii kwa uhuru, kuweko anga ya kiadilifu ya kunufaika na vyombo vya habari vya umma na iandae mazingira ya lazima na mwafaka kwa ajili ya kufanyika mazungumzo ya kitaifa na kufanyika uchaguzi wa wazi na katika mazingira huru na salama.

Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria

 

Ni kwa muda sasa Algeria imegubikwa na wingu la mgogoro wa kisiasa unaotokana na kutoridhishwa wananchi wa nchi hiyo na utendaji wa serikali. Katika hali ambayo, imepita zaidi ya miaka miwili tangu Rais wa zamani wa Algeria Abdelaziz Bouteflika aachie ngazi na hatamu za uongozi kushikwa na Rais Abdelmajid Tebboune, wananchi wa nchi hiyo wangali wanalalamikia utendaji wa serikali.

Akthari ya walalamikaji nchini Algeria wanaamini kuwa, uchaguzi wa Rais wa Disemba 12 mwaka 2019 ambao ulimleta madarakani Abdelmajid Tebboune kimsingi ulihuisha tu serikali ya zamani kwani viongozi wa zama za utawala wa Bouteflika kwa mara nyingine tena walifanikiwa kuchukua nyadhifa katika utawala mpya na hivi sasa wanaendeleza sera zile zile za huko nyuma.

Licha ya kuwa, Rais Tebboune akiwa na lengo la kujibu matakwa ya waandamanaji, katika miezi ya hivi karibuni amefanya mabadiliko ndani ya serikali, lakini kivitendo hakujafanyika mabadiliko katika wizara mbili muhimu na za kimsingi ambazo utendaji wake umekuwa ukikosolewa.

Abdelaziz Bouteflika, Rais wa zamani wa Algeria

 

Belkacem Zeghmati, Waziri wa Sheria wa Algeria ambaye amegeuka na kuwa nembo ya kamatakamata, kuwasaka wapinzani na wanaharakati wa harakati ya malalamiko na Ammar Belhimer, Waziri wa Habari na msemaji rasmi wa serikali ambaye anavidhibiti vyombo vya habari wameendelea kubakishwa katika nyadhifa zao licha ya malalamiko ya wananchi dhidi ya wizara hizo mbili.

Kuendelea malalamiko ya Waalgeria kulimlazimisha Rais Tebboune tarehe 18 Februari atangaze kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema Juni 12 mwaka huu.

Rais wa Algeria alisema katika tangazo lake kwamba: "Nimechukua uamuzi wa kulivunja Bunge na kuelekea kwenye uchaguzi usiokuwa na ufisadi ambao milango yake itakuwa wazi kwa vijana; na nimeazimia kutekeleza matakwa yote ya wananchi kuhusu marekebisho ya Katiba." 

Pamoja na tangazo hilo, Algeria imeendelea kushuhudia maandamano makubwa katika majuma ya hivi karibuni yanayolalamikia utendaji wa serikali.

Waliowengi nchini Algeria wanaamini kuwa, hatua hiyo ni ya kidhahiri tu na kwamba, mwisho wa siku haitayapatia ufumbuzi matatizo ya sasa.

Maandamano ya wananchi wa Algeria

 

Kuhusiana na suala hilo, Mabrouki Zeinuddin, mtaalamu wa Elimu Jamii anasema: Hatua kama kuvunja bunge na kufanya maandalizi ya uchaguzi wa mapema ambazo zilitangazwa na Rais Tebboune, hazina natija kwa wananchi wa Algheria ghairi ya mabadiliko ya kijuujuu tu na mbayo siyo ya kimsingi.

Wananchi wengi wa Algeria wanalalamikia mbinyo wa kisiasa na ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana katika maandamano ya wananchi hao kumekuwa kukisika nara kama: “Tunataka Algeria Huru na ya Kidemokrasia” na “Tunataka Nchi ya Kiraia na Siyo ya Kijeshi”.

Belkacem, mhadhiri wa Chuo Kikuu katika kitivo cha Sayansi ya Siasa anasema: Maandamano na malalamiko ya wananchi lengo lake ni kufikia mafanikio ambayo yataruhusu kuandaliwa mazingira ya kuweko mazungumzo ya kitaifa na serikali ya Algiers.

Waandamanaji nchini Algeria wanataka Rais Abdelmajid Tebboune ajiuzulu, kuweko vita vya kweli dhidi ya ufisadi, kuweko anga ya uhuru wa kisiasa na kiraia na kuboreshwa hali ya uchumi. Kadhalika wanataka kuendelea na madai yao hayo kupitia njia za kidemokrasia na bila ya utumiaji mabavu.

Kwa muktadha huo, malalamiko ya raia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika yataendelea kushuhudiwa. Kadiri tarehe ya kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge itakavyokaribia, basi ndivyo ambavyo tunapaswa kutaraji misimamo mingine ya vyama vya siasa na hatua nyingine kutoka kwa serikali.

Tags