Apr 07, 2021 07:38 UTC
  • Sudan yabatilisha sheria ya vikwazo na kuususia utawala haramu wa Israel

Baraza la Mawaziri la Sudan limebatilisha sheria ya vikwazo na kuususia utawala wa Kizayuni wa Israel, miezi michache baada ya Khartoum na Tel Aviv kuafikiana juu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili hizo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Baraza la Mawaziri la Sudan limesema katika taarifa iliyotolewa jana jioni kuwa, "tumepasisha dikrii ya kutengua sheria ya vikwazo dhidi ya Israel ya mwaka 1958."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, sheria hiyo ya kuondoa vizuizi vya ushirikiano na kufanya miamala na utawala pandikizi wa Israel itawasilishwa katika mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la Sudan na mawaziri hao kwa ajili ya kupata baraka za mwisho.

Kadhalika Baraza la Mawaziri la Sudan limedai katika taarifa hiyo kuwa, msimamo wa Khartoum kuhusu kuundwa taifa huru la Palestina katika fremu ya uundwaji wa mataifa mawili (Palestina na Israel) ungali thabiti.

Wasudan katika maandamano ya kupinga uhusiano na Wazayuni

Oktoba mwaka jana 2020, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilitangaza kuwa serikali ya mpito ya nchi hiyo imeafiki kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na hivyo kuifanya Sudan kuwa nchi ya tano baada ya Misri (1979), Jordan (1994), Imarati na Bahrain (2020) kufikia mapatano na Israel na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa Kizayuni.

Uamuzi huo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel unaendelea kupingwa na kulalamikiwa na makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Sudan, vikiwemo vyama washirika katika muungano unaotawala nchi hiyo.

Tags